kwamamaza 7

Burundi: Hatua ya kujiondoa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC)

0

Bunge nchini Burundi limeridhia kwa kauli moja na kupiga kura kujiondoa kwenye mkataba wa Roma unaoitambua mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC, kura iliyofanyika ikiwa ni siku chache tu zimepita toka umoja wa Mataifa uanzishe uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.

Muswada huo wa sheria uliungwa mkono na kupitishwa kwa kura 94, huku kura mbili zikikataa pendekezo hilo na wengine 14 hawakupiga kura.

Hii ina maana kuwa maamuzi ya bunge sasa yatapelekwa kwenye baraza la Seneti la nchi hiyo, ambalo nalo linaongozwa kwa sehemu kubwa na wabunge kutoka chama tawala, ambapo nao watapoga kura kabla ya kutiwa saini na rais kuidhinishwa rasmi.

Mwezi April mwaka huu, mwendesha mashataka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC, Fatou Bensouda, alitangaza ofisi yake kuanza uchunguzi wa awali kuhusu hali ya mambo nchini Burundi, ikiwa ni hatua ya kwanza kuelekea kufunguliwa kwa uchunguzi kamili na ikiwezekana kukamatwa kwa wahusika wa vitendo hivyo.

Ikiwa uchunguzi huo ungekamilika, basi mahakama ya ICC ingeanzisha uchaguzi rasmi kuhusu tuhuma za mauaji, mateso, mauaji ya kupangwa, ubakaji na watu kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha.

Uamuzi wa Burundi kujitoa kwenye mahakama ya ICC, unakuja wakati huu pia kukiwa na joto kubwa barani Afrika ambapo umoja wa Afrika nao kupitia wanachama wake, unataka nchi hizo zisishirikiane na mahakama hiyo pamoja na kujiondoa kwenye mkataba wa Roma.

Théogène U @Bwiza.com

Leave A Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.